Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) kesho (28 Februari 2017) atafungua mkutano wa siku moja wa Watendaji Wakuu na Wenyeviti wa Bodi za Mashirika ya Umma utakaojadili nafasi za Mashirika ya Umma katika utekelezaji wa Mpango wa II wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano.


Mkutano huu ulioandaliwa na Taasisi ya Uongozi kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina utafanyika Ikulu – Dar es Salaam kuanzia saa 2.30 asubuhi.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi Profesa Joseph Semboja amesema kwamba malengo ya mkutano ni kukusanya maoni ya viongozi kuhusu nafasi ya Mashirika ya Umma katika utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano; kuzungumzia changamoto tarajiwa katika utekelezaji wa majukumu haya na; kutoa mapendekezo ya namna ya kukabiliana na changamoto hizo.

“Mashirika ya Umma yana nafasi na uwezo mkubwa wa kufanikisha utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano, 2016/17–2020/21 wenye kaulimbiu ‘Maendeleo ya Viwanda kwa Mabadiliko ya Kiuchumi na Maendeleo ya Watu’,” alisema Profesa Semboja.

Profesa Semboja aliendelea, “Katika kuunga mkono jitihada za Serikali ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli mkutano huu unawakutanisha viongozi kutoka Serikalini na Mashirika ya Umma kwa lengo la kubadilishana maarifa na uzoefu wa jinsi mashirika haya yatakavyoiwezesha Tanzania kuwa nchi ya viwanda kwa maendeleo endelevu.”

Pamoja na mambo mengine, mkutano utajadili namna ya kuboresha mifumo ya  kiundetaji ndani ya mashirika na mahusiano miongoni mwa mashirika na taasisi za Serikali; kufungamanisha mipango ya mashirika ya Umma na Mpango wa Pili wa Maendeleo; kutathmini kiwango na aina ya rasilimali zinazohitajika kuwezesha utekelezaji wa mipango na; kufanya ufuatiliaji na tathmini ya mipango.

Mkutano utawakutanisha zaidi ya washiriki 100 kutoka Wizara, Mashirika ya Umma na Mamlaka za Udhibiti takribani 52 hapa nchini.

 Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano –Taasisi ya Uongozi.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...